Monday, January 7, 2013

MALECELA AZUNGUMZIA SAKATA LA GESI MTWARA-ASEMA LICHA YA KUSTAHILI KUWANUFAISHA WATANZANIA WOTE,UKIWA KARIBU NA WARIDI UNATAKIWA KUNUKIA

WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mwanasiasa Mkongwe nchini, John Malecela, ametoa wosia kuhusu mgogoro wa gesi akiiomba Serikali kufanya kila iwezalo ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mtwara wananufaika kwanza na rasilimali hiyo.
Malecela alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa na gazeti hili kutoa maoni yake kuhusu mgogoro wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam unaoendelea kushika kasi katika siku za hivi karibuni.
“Ukiwa karibu na waridi unatakiwa kunukia waridi. Wakazi wa Mtwara nao wanatakiwa wanukie waridi,” alisema.
Malecela alisema, pamoja na ukweli kwamba rasilimali inayopatikana nchini ni kwa ajili ya watanzania wote, ukweli kwamba wakazi wa eneo inakopatikana rasiliamali hiyo wanapaswa kunufaika nayo, haukwepeki.
“Hatutakiwi kuwaacha hivi hivi wana-Mtwara eti kwa sababu hii ni rasilimali ya Watanzania wote. Ni lazima wanufaike zaidi, wao kuliko wengine kwa kuwa wako karibu na waridi,” alisema Malecela.
Alisema licha ya gesi hiyo kuwa ya watanzania wote, Serikali inatakiwa kuandaa utaratibu ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Mtwara wananufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Malecela alieleza kuwa umaskini uliokithiri katika baadhi ya mikoa nchini ukiwamo mkoa wa Mtwara, ndio unaosababisha watu waanze kudai rasilimali zinazotoka katika maeneo yao wakiamini kuwa ndio mwanzo wa ukombozi wao.
“Serikali iyaangalie kwa umakini maeneo yanayotoa utajiri na rasilimali, ni lazima wapewe upendeleo ili wafurahie matunda mali asili yao,” alisema Malecela.
Kuhusu gesi kutoka Mtwara
Malecela alisema anaunga mkono gesi kusafirishwa mahali popote palipo na soko kubwa ili iweze kuwanufaisha Watanzania lakini, lazima kuwe na mkakati wa kuwanufaisha pia wakazi wa eneo husika.
“Mnaweza kuisafirisha gesi kwenda mahali popote palipo na soko kubwa, lakini mkaangalia namna mnavyoweza kuwanufaisha wakazi wa Mtwara,” alisema na kuendelea;
“Rasilimali  inayogundulika popote ndani ya Tanzania ni mali ya watanzania wote, hivyo hata gesi ya Mtwara si ya wakazi wa Mtwara peke yao.”
“Kama ilivyo kwa bwawa lililopo katika Jimbo la Mtera linalozalisha umeme na kuingizwa katika gridi ya taifa kwa ajili ya watanzania wote,  gesi nayo inatakiwa kuwanufaisha watanzania wote,”
Mkazi Mtwara atishia gesi kutoonekana
Katika hatua nyingine Kikongwe Somoe Issa (90) ambaye ni mkuu wa kaya ya Msimbati, kijiji ambacho gesi asilia inavunwa ameionya Serikali kutoendelea na mpango wake wa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam na kwamba iwapo itapinga bomba hilo litasafirisha maji badala ya gesi.
Kikongwe huyo ambaye haoni wala kusikia alisema hayupo tayari kuona gesi hiyo ambayo imepatikana katika kijiji hicho ikiondoka mkoani Mtwara.
“Atakayejaribu kuondoa gesi hii kitakachomkuta atakijua yeye mweyewe…ninasema gesi isiende kokote…iwapo atabisha inawezekana akasafirisha maji tu na isiwe gesi yenyewe” alisema bibi huyo kupitia kwa mkalimani wake Asha Hamis
Aliongeza kuwa,“mwaka walioanza kuchimba (2005) walifika hapa bila kubisha hodi, wanajua kilichowakuta…bomba lilikuwa haliendi chini wala kurudi juu…walinifuata hapa nikaenda kufanya tambiko”
KUTOKA MAGAZETI YA LEO

No comments:

Post a Comment