SERIKALI ya Malawi imesema ina wasiwasi kuhusu hatma ya mgogoro
wa mpaka wa Ziwa Nyasa na kwamba hali hiyo inatokana na Tanzania kuvunja
sehemu ya makubaliano ya usuluhishi.
Kauli hiyo inakuja wakati jopo lo viongozi
wastaafu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika(Sadc), likijiandaa kuwasilisha ripoti yake baadaye mwezi huu.
Jopo hilo linaloongozwa na Rais Mstaafu wa
Msumbiji, Joachim Chissano, litakabidhi ripoti hiyo kwa viongozi wakuu
wa nchi zote mbili.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Malawi, Ephraim
Chiume, ameituhumu Tanzania kwamba imeanza kuzungumzia utatuzi wa
mgogoro huo wakati ikijua kuwa mzozo huo uko katika hatua ya upatanishi
maalumu.
Waziri Chiume aliikosoa kauli iliyotolewa hivi
karibuni na Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka baina ya mataifa hayo
mawili, unakaribia kupatikana.
Alisema kitendo cha Membe kuzungumzia maendeleo
ya mgogoro huo kinapingana na makubaliano ya pamoja yaliyowasilishwa
kwa Chissano na kwamba hatua hiyo inavunja moyo.
Waziri Chiume aliliambia gazeti la Nyasa Times
kuwa pande zote mbili zilipokutana Nombemba 17 mwaka jana jijini Dar es
Salaam, zilikubaliana kuzungumzia mgogoro huo ili kuepuka kuingilia
juhudi za upatanishi.
Alisema hata hivyo, hivi karibuni ya Serikali ya Tanzania imekiuka sehemu ya makubaliano hayo.
“Tanzania wamevunja makubaliano, na sisi tunasisitiza kuwa Ziwa Nyasa ni la Malawi,” alisema waziri.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo, wamesema kauli huyo
inaashiria kuwa huenda pande hizo mbili zikashindwa kukubaliana na
mapandekezo yatakayowasilishwa na mpatanishi wa mzozo huo.
Mpatanishi huyo mwezi huu anatazamiwa kukutana na Rais Jakaya Kikwete na yule wa Malawi, Joyce Banda.
Hata hivyo, alivyotafutwa ili kuzungumzia
malalamiko hayo, waziri Membe kupatikana, lakini Naibu wake Mahadhi
Maalimu, alisema: “Ninachosema mimi kwanza hizo taarifa sijazipata na
kama zipo basi Serikali itawasiliana kupitia mikondo sahihi. Serikali
haiwezi kujibizana kupitia magazeti”
No comments:
Post a Comment