Jinsi ya kuwaelewa bayana watoto na
kuboresha ukaribu baina yetu na wao.
1. Faida/Manufaa
ya Kuwa karibu na Watoto:
Yako manufaa na faida nyingi kwa
sisi kuwa karibu na watoto.
Watoto wanaweza kukufanya kuhisi umuhimu fulani na kuhitajika wakati wote
na wao. Mara zote hukubali madhaifu yetu
na kuyashangilia yale wanayoyapenda kutoka kwetu.
Ni watu wa kusamehe kwa urahisi sana, kamwe hawawezi kuficha
wanachofikiri au kukihisi, uwazi wao huu ni faida kwetu ingawa mara nyingine
watu wazima wengine hukasirika. Ukweli
ni kwamba uwazi wao kwetu haumaanishi kutuumiza au kutuumbua.
Ni faida kubwa kwetu pale tunapoona ukaribu wetu na mtoto au watoto fulani
unabadilisha maisha au tabia zao.
Kupitia jitihada zako watoto wanaweza kujifunza kujitegemea, ushirikiano,
mambo ya afya, kupendana n.k.
Watoto wa leo wengi wanaishi au kupitia katika familia zenye mazingira
magumu sana, mfano: Familia zenye ulevi, unyanyasani, talaka na kutengana,
matatizo ya kiuchumi. Watoto hawa
wanahitaji kutiwa moyo kuliko wale wenye hali njema. Utajisikia faraja sana pale utakaposaidia kwa
namna moja au nyingine mtoto mmoja kuifikia hatima yake vema.
Kuwa karibu na watoto hutuwezesha kubakia ujana hasa katika fikra
zetu. Hali ya kuutazama ulimwengu na maisha
kama mtoto anavyotazama hutupa kupunguza au kuondokana na misongo ya mawazo ya
maisha. Tunajikuta tunafurahia kila kitu
kama vile watoto wafanyavyo, hapa tunasema “Yatazame maisha katika jicho la mtoto”.
Kwa kuwa karibu na watoto tunapata nafasi ya kutambua vipawa vyetu, hasa
vile vilivyojificha na kuviweka katika utendaji kwa manufaa ya watoto, sisi
wenyewe, na jamii nzima kwa ujumla.
Hata kama ukaribu na watoto ilikuwa ni ngumu kwako, taratibu
utakapojaribu itafukua upendo wa kweli toka moyoni mwako na mara utatamani kuwa
karibu na kujifunza kutoka kwao.
2. Changamoto
Zilizopo:
·
Kwa wengi, inaonekana kabisa kuwa, kuwa karibu
na watoto mara nyingi huchosha hisia, akili, mwili na hata kusababisha msongo
wa mawazo mara nyingine. Hii huwa ngumu
zaidi pale ambapo huna upendo wa dhati kwa watoto.
·
Baadhi ya mahitaji au misaada ambayo hatuna budi
kuifanya tunapokuwa na watoto hutupa changamoto na wengine huona ni kinyaa au
uchafu.
·
Mara nyingine yaweza kuwa rahisi kuambukiza
baadhi ya magonjwa madogo madogo kama mafua, kikohozi, ndui n.k. au wewe
kuwaambukiza wao pia.
·
Mara nyingine kuwa karibu na wato
hutugharimu. Ziko nyakati ambazo
watataka kitu ambacho kinahitaji kununuliwa kwa fedha, au waweza kulazimika
kutumia muda wako kufanya matakwa yao.
·
Ziko nyakati watoto hupitia magumu katika
familia zao na hali hii huweza kuathiri tabia au hisia zao nahii kuwa
changamoto kwa yule aliyekaribu nao.
Mfano magonjwa ya muda mrefu kwa mzazi au wazazi, vifo, kutengana kwa
wazazi n.k. hivi vyote vyaweza kuathiri hisia na tabia za mtoto.
Mambo yatakayo tuwezesha kuboresha
ukaribu / urafiki baina yetu na watoto:
1. Kuwakubali
na kuwapenda watoto (Appreciation)
Ni ngumu kabisa kuwa karibu na watoto na kutafuta kukubalika nao pasipo
kwanza kuwakubali. Mawasiliano yako na
wao yanatakiwa kuwa ya kiwango cha juu kuliko yale unayofanya na watu
wazima. Kama ni mzazi, tamani au tafuta
kuutumia muda unapokuwa na watoto vizuri.
Wape muda na wewe kadri inavyowezekana.
Shiriki nao katika baadhi ya yale wanayoyafanya. Washirikishe pia katika yale unayodhani
watapenda kuona ukiyafanya. Usiwaangalie
tu au kuwaacha wakutazame ukifanya.
Kumpakata mtoto wakati wa hadithi ni mfano wa kushiriki nae. Hii hujenga mahusiano mazuri sana kwao.
2. Kuwa
tayari kutumia nguvu zetu au nishati yetu ya mwili kwa ajili yao
Watoto huwa na nishati au nguvu nyingi katika vile wanavyovifanya. Hali kadhalika mtu anayetamani kuwa karibu
nao ni lazima awe tayari kutumia nguvu zake katika kushiriki nao. Mfano, watapenda kukimbizana, watapenda kuruka,
au kutembea haraka na michezo mingine mingi.
3. Kuwa
na hali nzuri ya utu (Sense of humor)
Hali hii huwafanya watoto kukuona wewe ni sawa nao. Watoto hupenda sana pale unapokuwa tayari
kucheka na kuwa na hisia kama walizonazo.
Najua unahitaji muda wa kuwaza juu ya biashara au kazi zako, na watoto
nao kwa upande mwingine wanataka muda ambao hutawaza yalio yako bali yaliyo yao
tu.
Mara nyingine, watoto hufanya vitu vya kuchekesha, tunachotakiwa ni
kucheka nao na sio kuwacheka. Hii
itaepusha kuwaumiza moyo.
4. Uvumilifu
(Patience)
Uvumilivu ni muhimu sana kwa yeyote anayetaka kuwa karibu na watoto. Watoto hufanya makosa mengi, na pia ni
wataratibu katika kufanya mambo maana ujuzi wao bado ni mdogo. Kwanza ndio wanajifunza kujitawala na kufuata
maelekezo na pia wanahitaji kukumbushwa mara kwa mara. Ni wakati wa kuulizwa maswali mengi na ya
marudio, hata yale yasiyo muafaka.
5. Kuwa
na huruma (Compassion)
Huruma kwa watoto huambatana na uvumilivu. Mtu mwenye huruma ni yule anayetambua pale
mwenzake anapokuwa na tatizo au uhitaji na yuko tayari kutoa msaada. Watoto humwitaji mtu anayewaelewa na kujali
mahitaji yao. Vipo vitu ambavyo vyaweza
kuonekana vidogo na vya kawaida kwetu, kumbe kwa watoto ni vikubwa na vyenye
kuwaogopesha sana. Tunategemea huruma na
kujali kwako kutaongezeka hasa kwa wale watoto wenye matatizo au uhitaji mkubwa
mfano: watoto wenye magonjwa ya kudumu, ulemavu au matatizo ya kifamilia.
6. Kuwa
mtu unayekubali mabadiliko (Be flexible)
Watoto wako tofauti sana na huwezi kuwa tabiri, mara nyingine watataka
kitu fulani na mara hubadilika. Hawana
muda wa kufikiri athari au usumbufu wa kubadilika au kubadilisha maamuzi
yao. Kwa sababu ni vigumu kufahamu ni
nini kitajiri kwa mtoto baada ya muda mfupi ujao basi ni lazima tuwe tayari
kubadilika. Pasipo hili basi utakuwa na
wakati mgumu sana kuwa rafiki wa watoto.
7. Kuwa
Mgunduzi (Be creative)
Mtu mwenye mawazo na fikra za kigunduzi atapata urahisi sana katika kuwa rafiki
wa watoto. Jaribu kuwa mpya kwa watoto
kila mara, sio kila kitu unachofanya
kwao kiwe ni kile kile siku zote. Amsha
hamasa yao kwa vitu, mambo au mawazo mapya mawakati wote. Watoto hawapendi kufanya kitu fulani kwa njia
au mfumo uleule kila wakati.
8. Kuwa
mtu wa watu na mpenda watu (Be sociable)
Watoto huwa wanatusoma sana, pale unapojaribu kuwa mwema kwao, kucheka
nao na kuwa karibu nao na wakati hauko hivyo kwa wengine ndani au nje ya familia
yako unawafanya wasikuelewe na taratibu huanza kukuhofu.
Waruhusu wakuone ukiwa halisi, hususani unapohusiana na wao pamoja na
wengine pia.
Wazazi au mzazi anayependa kujitenga na kuwa mpweke hupata shida sana katika
kuwafanya watoto kuwa karibu nae.
9. Maanisha
na ujitoe kwao (Be committed)
Wakati unapoamua kufanya kitu na watoto au mtoto, basi maanisha. Usiwe na vitu vingi wakati mmoja. Wape nafasi yao na iwe yao peke yao.
Jitoe kufanya vema uwezavyo katika kuhakikisha unawajali na kuwafurahisha
watoto. Watoto pia hufurahi sana pale
wanapoona umetoa moyo wako wote kwa ajili yao. Kama umeamua kuanza kitu nao
basi malizia, usikiachie katikati.
Kama unajua au kuhisi kwamba hutomaanisha katika lile unalolifanya ukiwa
nao basi ni bora uache mpaka pale utakapojiona kuwa utamaanisha.
Imeandaliwa
na:
Chris
Mauki
Mtaalamu
wa mahusiano na ushauri wa kisaikolojia
University
of Dar es salaam
No comments:
Post a Comment