Thursday, November 14, 2013

MENO YA TEMBO ZAIDI YAKAMATWA KATIKA KONTENA BANDARINI ZANZIBAR

Kwa mara nyingine katika kipindi kisichozidi wiki mbili, polisi nchini Tanzania wamenasa shehena kubwa ya meno ya tembo yakiwa yamefichwa katika kontena, bandarini Zanzibar.
Watu wawili wamekamatwa wakihusishwa na meno hayo.Kamishna Mussa amesema, kwa sasa kiasi hicho cha meno ya tembo bado hakijafahamika kutokana na kuendelea kwa kazi ya kupakua kutoka kontena hilo.Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, meno hayo yalikuwa yamehifadhiwa katika kontena la futi arobaini yakiwa yamechanganywa katika mifuko iliyohifadhi makombe ya konokono wa baharini, tayari kwa kusafirishwa nje.
Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.
Kukamatwa kwa meno haya ya tembo, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.
Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18 sawa na dola zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.

No comments:

Post a Comment