Monday, December 31, 2012

MBEYA:Moto wateketeza tena mali Soko la Mwanjelwa

BIDHAA mbalimbali zenye thamani zaidi ya Sh2 bilioni na gari moja, zimeteketea kwa moto baada ya ghala kuu la wafanyabiashara wa Soko la Mwanjelwa na Sido kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.
Hilo ni tukio la tatu kwa soko hilo kuungua moto. Mara ya kwanza ilikuwa Desemba 2006, baada ya soko hilo kuteketezwa na moto na wafanyabiashara kuhamishiwa eneo la Sido ili kupisha kujengwa upya.
Moto mwingine ulizuka tena sokoni hapo Septemba mwaka jana na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 20 kujeruhiwa huku mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zikiteketea.
Katika tukio la juzi, moto huo ulioanza juzi usiku saa 2:30 na kuzimwa majira ya saa kumi na moja alfajiri, unadaiwa kuwa chanzo chake ni hujuma.
Mkurugenzi  na mmiliki wa ghala hilo, Erasto Sanga (Usagatikwa) alisema alipata taarifa ya ghala lake kuwaka moto kutoka kwa msamaria mwema saa tatu usiku... “Nilipofika hapa nikakuta chumba cha kampuni ya Jambo ambao ni wapangaji wangu kinawaka moto ndipo nikaanza kufanya mawasiliano na zimamoto.”
“Hawa wapangaji wangu hawana tabia ya kufungua ofisi saa moja usiku, lakini jana walifika na kufungua chumba chao na baadaye kuondoka. Walipoondoka ndipo moto ulipoanza kuwa katika chumba chao,” alisema na kuongeza:
“Mali yangu iliyoharibika ina thamani zaidi ya Sh600 milioni na hatua niliyochukua ni kutoa taarifa hizi polisi na nimewaachia wafanye kazi yao,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alisema moto huo umeteketeza vyumba vitatu vya wafanyabiashara, vilivyokuwa na bidhaa mbalimbali na watu wawili wanashikiliwa kwa madai ya kuiba mali na kuzuia magari yasiingie kuokoa mali.
Kamanda Athumani alisema kulikuwa na kundi la watu ambalo lilikuwa linawapiga mawe waokoaji na polisi.... “Nimesikitishwa sana na kundi la watu wachache wanatumia njia ya matatizo kama haya kujinufaisha kwa kufanya uhalifu wa kuiba mali za watu na wengine... walidiriki hata kuwapiga mawe waokoaji na polisi na kulizuia gari la Zimamoto lisiingie ndani kwa kuweka mawe barabarani.”
Hata hivyo, alisema wananchi na askari hao walifanikiwa kuokoa magari yapatayo saba yaliyokuwapo nje ya ghala hilo kwa kuyasukuma.

No comments:

Post a Comment