Tuesday, February 12, 2013

Dk Salim, Nchimbi, Tibaijuka waula CCM

HARAKATI za kupanga safu za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimehitimishwa usiku wa kuamkia leo baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kuchagua wajumbe wa Kamati Kuu (CC).
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao cha NEC jana, walioula kuingia katika chombo hicho kikuu cha uamuzi ndani ya CCM ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim na mawaziri kadhaa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Dk Salim ambaye aligombea urais dhidi ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, aliteuliwa jana kuwa mjumbe wa NEC na baadaye jina lake kupendekezwa kuwa miongoni mwa waliopigiwa kura za kuwa wajumbe wa CC.
Makada 14 wa CCM, saba kutoka kila upande wa muungano walipigiwa kura katika uchaguzi huo ambao matokeo yake yalitangazwa usiku wa manane.
Kutoka Tanzania Bara, waliochaguliwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na Mbunge wa Viti Maalum, Pindi Chana.
Kutoka Tanzania Zanzibar mbali na Dk Salim, wengine ni Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi.
Pia wamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Maua Abeid Daftari pamoja na  Khadija Aboud.  Wajumbe hao wapya wanaunda Kamati Kuu pamoja na wengine wanaoingia kwa nyadhifa zao.
Vigogo urais watoswa
Uteuzi wa makada waliopigiwa kura uliwaweka kando vigogo ambao wamekuwa wakitajwa kuusaka urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015.
Miongoni mwa waliowekwa kando ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mawaziri waandamizi wawili katika Serikali ya Rais Kikwete, Samuel Sitta (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).
Kadhalika, majina makubwa ndani ya chama hicho kama vile January Makamba, Martin Shigela, Willison Mukama, Mohamed Seif Khatib, Omar Yusufu Mzee na wengineo hayakuwamo kwenye orodha ya waliopigiwa kura.
Baadhi ya makada walioanguka Balozi Ali Karume, Gwaride Jabu, Dk
Raphael Chegeni, Dk Cyril Chami, Michael Lekule Laizer, Ramadhan Madabida, Hassan Wakasuvi, Dk Fenella Mukangara, Shamsa Mwangunga na Said Mtanda.

No comments:

Post a Comment