HUYU NDIE MTANZANIA ALIEJIPATIA UWAZIRI HUKO UGAIBUNI
RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba
kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika
Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara
nyingine mpya.
Mdogo wa Profesa
Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam, alisema ndugu
yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani
Kagera.
Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia
wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka
yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake
sisi kama wanafamilia.”
Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM),
Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika
chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.
“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza
Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo
Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.
Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame
ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali
kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya
wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.
Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa
miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo
lililomfurahisha Rais Kagame.
Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya
kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo
alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.
Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa
Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.
Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata
Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu
katika fani hiyohiyo.
No comments:
Post a Comment