Matokeo yake ni kuzidi kudidimia kwa uchumi
kutokana na mgao huo kuathiri shughuli nyingi za kibiashara na sekta
nyingine nyingi zinazochangia pato la taifa. Hii ni baada ya Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kutangaza mwaka jana kwamba
mgao wa umeme hapa nchini ungekuwa jambo la historia.
Lakini kwa muda mrefu sasa maswali yamekuwa
yakiulizwa kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara. Kwa miaka mingi sasa
Tanesco imekuwa ikitoa visingizio vinavyojirudia na kuonekana
vimetolewa mahsusi kuwaghilibu wananchi.
Visingizio hivyo ni pamoja na kukata miti kwenye
njia za nyaya za umeme, kubadilisha nguzo zilizooza, kubadilisha au
kukarabati transfoma.
Kukataa kuwafahamisha wananchi kuhusu kuwapo kwa
mgao na sababu zinazosababisha mgao huo kumewakwaza wananchi, kwa maana
ya kutoweza kujipanga vizuri katika shughuli zao mashuleni, vyuoni,
majumbani, maofisini, viwandani na katika biashara mbalimbali kama
saluni, mabucha na magereji.
Shughuli hizo zimekuwa zikivurugika kutokana na
Tanesco kutoweka ratiba ya mgao wa umeme ili wadau wapange shughuli zao
kutokana na ratiba hiyo.
Waswahili waliposema mficha maradhi kifo
humuumbua, walipatia kabisa usemi huo, kwani Tanesco ambayo imekuwa
ikificha matatizo yake na kutoa visingizio lukuki, jana ilitoka
mafichoni na kutangaza kwamba inakabiliwa na hali mbaya kifedha, ikiwa
ni pamoja na kulemewa na madeni.
Hatua hiyo ya Tanesco haikuwashangaza wengi.
Sisi tumekuwa miongoni mwa wengi ambao tumekuwa
tukisema shirika hilo livunjwe na kusukwa upya kutokana na muundo wake
kutoweza kuleta ufanisi, huku likikwamishwa na vitendo vya ufisadi na
hujuma za viongozi na wafanyakazi.
Ni siri iliyo wazi sasa kwamba hali mbaya kifedha
imesababisha makampuni yanayozalisha umeme kutishia kusitisha uzalishaji
umeme. Tanesco haikopesheki na ndiyo maana ilikosa dhamana ya kukopa
benki Sh408 bilioni mwaka jana na sasa inategemea ruzuku ya Serikali.
Makampuni yanayozalisha umeme yanaidai Tanesco Sh5.4 bilioni kila siku wakati shirika hilo linakusanya Sh2 bilioni tu kwa siku.
Hiyo ndiyo hali halisi ya Tanesco ambayo imekuwa
ikiendesha shughuli zake kwa kupandisha bei ya umeme kila mwaka.
Serikali sasa imelikatalia kupandisha bei ya umeme. Je, shirika hili
lina uhalali wa kuendelea kuwapo? chanzo gazeti Mwananchi
No comments:
Post a Comment