Dodoma. Spika wa Bunge, Anne Makinda jana ni kama aliruhusu
mvutano wa wazi baina ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa
Chadema ambao kila upande uliutuhumu upande mwingine kwa kuhusika kwa
viendo vya ugaidi.
Licha ya kutozungumzia suala hilo moja kwa moja,
lakini msingi wa tuhuma hizo ni kesi iliyofunguliwa mahakamani dhidi ya
Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Willifred Lwakatare ambaye anakabiliwa
na makosa yanayomtuhumu kwa ugaidi.
Katika mazingira hayo ni dhahiri wabunge
waliingilia uhuru wa mahakama kwani kesi husika iko mahakamani na Spika
Makinda katika moja ya miongozo yake jana alisema: “Itabidi Kamati ya
Kanuni ikutane kwa kuwa mambo yanayozungumzwa yako mahakamani, hivyo ni
muhimu mahakama ikaheshimiwa.”
Kifungu cha 114 (1) cha Sheria ya Kanuni za adhabu
(Penal Code), kinatoa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela kwa mtu
yeyote ambaye kwa namna yoyote anatoa matamshi yenye mwelekeo wa
kushawishi uamuzi wa mahakama kwa suala lolote ambalo liko mahakamani
likisubiri uamuzi.
Matamshi hayo ni yale yenye mwelekeo wa kupindisha
mwenendo wa kesi husika au yenye mwelekeo wa kutaka uamuzi upendelee
upande fulani au matamshi yenye lengo la kudhalilisha au kushusha hadhi
ya mamlaka ya mtu ambaye kesi yake iko mbele ya mahakama.
Mjadala kuhusu ugaidi ulianza kuchipua juzi wakati
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alipowasilisha maoni ya
kambi yake kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu kwa kusema: “Umeibuka uchochezi
mpya wa kisiasa wenye ubia kati ya chama tawala na vyombo vya dola na
kinachoitwa ugaidi.”
Mbowe alisema kambi yake inashangazwa na uhodari
wa Serikali katika kuchukua hatua kwa suala la mtu aliyebambikiwa kesi
ya ugaidi kwa ushahidi wa kughushi kuwa yeye ndiye gaidi.
“Kambi yetu inasikitika sana kuona wale wote
waliokuwa wakiwasiliana na hao wanaoitwa magaidi ambao pia ni viongozi
wa CCM na washirika wao hawajachukuliwa hatua yoyote,” alisema Mbowe na
kuongeza:
“Tunaulaani mkakati huu wenye nia ovu ya kufifisha
demokrasia hapa nchini...mpango huu haramu hautafanikiwa ... na hili
nalo likiachiwa likakomaa litaliingiza Taifa letu katika hatari nyingine
ya machafuko.”
Jana suala hilo lilichukua sura ya kisiasa zaidi
pale wabunge wawili; Mwigulu Nchemba wa Iramba Magharibi (CCM) na Tundu
Lissu wa Mbunge wa Singida Mashariki walipochangia hotuba hiyo na kuzama
katika eneo la ugaidi, hali iliyosababisha mvutano mkali bungeni.
Kauli ya Nchemba
Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM
(Tanzania Bara) aliishambulia hotuba ya Mbowe akieleza kuwa hakuna haja
ya kuhangaika na suala la ugaidi kwa kuwa Chadema ndiyo wanahusika nalo
kwa kupanga kumdhuru mwandishi wa habari.
“Watu wanapanga ugaidi halafu wanaachiwa tu, nashukuru Mbowe
hayuko hapa nadhani atakuwa amekamatwa pamoja na katibu wake kwa kuwa
wao ndio wamekuwa wakiwasiliana na aliyekuwa amepanga ugaidi,” alisema
Nchemba.
Alisema viongozi hao wanapswa wakamatwe na
kuunganishwa kwenye kesi ya ugaidi kwa kuwa haiwezekani wakapanga mauaji
ya mwandishi halafu wakaachwa hivihivi.
“Aliyerekodi video ya mipango ya ugaidi yupo na
alikuwa pia akiandika na taarifa yake ipo, hivyo wajue tu kwenye hili
suala la ugaidi sitakaa kimya,” alisema Nchemba.
Baada ya Nchemba kumaliza Mbunge wa Mbulu,
Mustapha Akonaay aliomba mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 68(2)
kwamba jambo ambalo limezungumzwa na Nchemba tayari liko mahakamani
hivyo ni kinyume na sheria.
Spika Makinda alijibu akieleza kuwa suala hilo
tayari lilishazungumzwa na Mbowe hivyo ni lazima wote wafuate sheria na
kuongeza: “Isiwe ni mkuki kwa nguruwe.”
Katikati ya majadiliano alisimama Mbunge wa Viti
Maalumu (Chadema), Pauline Gekul na kutaka mwongozo wa Spika kuhusu
Nchemba kutukana na kiti chake kukaa kimya.
Spika Mkinda alijibu akisema, “Jana hotuba nzima
ya kiongozi wa upinzani tulinyamaza, hivyo hivyo tunyamaze, tunaendelea
na ninaomba watu wafuate utaratibu.”
Lissu ajibu
Hata hivyo baadaye Lissu ambaye pia ni Mwanasheria
wa Chadema aliposimama kuchangia hotuba hiyo alisema kuna watu
wamemlipa mtu fedha za kufanya ugaidi na mmoja wa watu hao ni mheshimiwa
ambaye yupo bungeni.
“...Kuna mheshimiwa humu ndani aliwasiliana na
gaidi,” alisema Lissu kabla ya Anne Abbdalah kumtaka athibitishe na
Lissu alisema: “Ushahidi upo kama Anna Abadallah anataka, kwani malipo
yalifanywa na magaidi waliopo humu ndani..”
No comments:
Post a Comment