Mabalozi 12 wa Umoja wa Ulaya (EU), nchini wamemtumia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda barua ya wazi wakimtaka kuchukua hatua stahiki kwa watu waliofanya mauaji ya albino wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.
“Tumesikitishwa na mauaji ya kikatili ya albino Munghu Lugata yaliyotokea Mei 12, 2014 wilayani Bariadi,” ilieleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na mabalozi 12 wa nchi wanachama wa EU Tanzania, wakiongozwa na Balozi wa Umoja huo nchini, Filiberto Sebregondi.
Mabalozi wengine waliosaini barua hiyo ni Dianna Melrose wa Uingereza, Koenraad Adam wa Ubeligiji, Johnny Flento wa Denmark, Sinikka Antila wa Finland, Marcel Escure wa Ufaransa, Fionnuala Gilsenan wa Ireland, Luigi Scotto wa Italia, Jaap Frederiks wa Uholanzi, Luis Manuel Cuesta Civis wa Uhispania, Lennarth Hjelmaker wa Sweden na Kaimu Balozi wa Ujerumani, Hans Koeppel.
Katika tukio hilo linalohusishwa na ushirikina, watu wasiofahamika walimuua Lugata na mwili wake ulikutwa nje ya nyumba yake ukiwa umejeruhiwa vibaya.
Barua hiyo ilisema kuwa Pinda amekuwa mstari wa mbele kupambana na vitendo hivyo, bila shaka atahamasisha mamlaka za chini yake kuchukua hatua za kisheria.
“Tunakuomba kwa mara nyingine kuhamasisha mamlaka zako kutokomeza vitendo hivi vya kikatili kwa kuhakikisha havijirudii tena na kufanya uchunguzi makini na kuwafungulia mashtaka wale wote waliohusika,” ilisema.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Lugata ni albino wa 73 kuuawa nchini tangu mwaka 2000 na wa kwanza kwa mwaka 2014.
Katika barua hiyo ambayo pia ilithibitishwa na Mkuu wa Idara ya Siasa, Habari na Mawasiliano ya EU, Tom Vens, mabalozi hao 12 wanafahamu fika kuwa waganga wawili wa jadi wanahusika katika mauaji hayo.
Wakati huohuo; Ubalozi wa Uingereza nchini umezungumzia suala la uchunguzi wa uchotaji wa zaidi ya Sh200 bilioni katika Akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ukisisitiza kuwa suala hilo lishughulikiwe ipasavyo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pia ubalozi huo umekanusha madai ya balozi wake nchini kuhusika katika mkakati wa kujaribu kukwamisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa jana, ilieleza kwamba unafuatilia kwa karibu kuhusu taarifa za ubadhirifu uliofanywa kupitia Kampuni ya IPTL, ikihusisha Akaunti ya Escrow na BoT, lakini hauna sababu ya kuingilia kukwamisha bajeti ya Wizara ya Madini kama ilivyotajwa na baadhi ya vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment