Monday, June 16, 2014

Watu 48 wafariki katika shambulizi Kenya


Watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Al Shabaab wameshambulia kituo cha polisi na hoteli mjini Mpeketoni, pwani ya Kenya .
Makabiliano makali yameripotiwa sehemu kubwa ya Jumapili usiku huku wakaazi wakitorokea msituni karibu na kisiwa cha Lamu. Shirika la msalaba mwekundu linasema kuwa hadi kufikia sasa watu 48 wanahofiwa kuuawa katika shambulizi hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo. Hata hivyo vyombo vya habari vinasema idadi hiyo huenda ikawa juu zaidi. Shambulizi lilifanyika usiku wa kuamkia leo pale ambapo watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakiwa wamejihami vikali walivamia vituo vya polisi , hoteli na benki. Shambulizi hilo linakuja siku kadhaa baada ya serikali ya Uingereza kufunga ofisi zake mjini Mombasa kwa hofu ya usalama. Duru za jeshi la Kenya zimearifu kuwa wapiganaji hao hawajajitambulisha ni wa kundi gani.


Kituo kimoja cha polisi kilichoshambuliwa na wapiganaji hao Baadhi ya walioshuhudia wamearifu kuwa 
wameona maiti kadhaa na majeruhi wengi japo Polisi hawajathibitisha ni watu wangapi wameuawa.Kenya 
imekumbwa na mashambulio kadhaa kutoka kwa wapiganaji wa kisomali wa Al Shabaab tangu ipeleke 
wanajeshi wake ndani ya Somalia mwaka wa 2011.Duru kutoka kisiwa cha Lamu zimearifu kuwa wapiganaji hao walifika katika malori mawili na kurusha kifaa kama bomu ndani ya kituo cha polisi kisha wakakivamia na kuiba silaha.
'Washambuliaji ni kina nani ?'
Msemaji wa Jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir ameandika katika mtandao wa Twitter kusema kuwa wapiganaji hao wameshambulia kijiji kimoja na kufyatua risasi kiholela katika kituo kikuu cha biashara.''Huenda wapiaganaji hao wakawa Al shabaab,'' ameongeza Meja Chirhir.Mmoja wa walioshuhudia amesema kuwa hoteli zilishambuliwa. "Baadhi ya hoteli zimewashwa moto hatujui watu wangapi wamejeruhiwa kufikia sasa. Tumeambiwa wameshatoroka lakini polisi wanawafuata waliko,'' alisema mtu huyo

No comments:

Post a Comment