Thursday, November 8, 2012

Ikulu: Hatuwezi kumzuia Lissu kumshtaki Rais:Kwahisani ya Gazeti Mwananchi


Sehemu ya 11 ya Kanuni ya Bunge, Ibara ya 121 inaeleza kuwa mbunge yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya hoja ya kumshtaki Rais kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kupitia azimio la Bunge kwa mujibu wa Ibara  ya 46 A ya Katiba ikiwa inadaiwa kwamba Rais; ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja katiba au sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Gedius Rwiza
SIKU moja baada ya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu kusema atawasilisha hoja ya kumshtaki Rais Jakaya Kikwete iwapo atashindwa kuwaondoa kazini majaji wasio na sifa aliowateua, Ikulu imemwambia aendelee na mchakato wake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana kuwa hakuna anayemzuia Lissu kushtaki kama anaona kuna sababu za kufanya hivyo.“Lissu ni Mbunge na ana haki zake za msingi na kama amefikia hatua hiyo anaweza kufanya hivyo... hakuna mtu ambaye anaweza kumkataza. Nani mwenye uwezo wa kuingilia uhuru wa mtu?”Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge jana, Lissu alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona Bunge limeikalia ripoti ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomhoji kuhusu kauli yake ya kuwatuhumu majaji kuwa baadhi yao hawana sifa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona Rais Kikwete ambaye ana mamlaka ya kuteua majaji, ameshindwa kuwaondoa kazini majaji hao wasiokuwa na sifa.
Lissu alisema atawasilisha hoja yake hiyo kwa kutumia Kanuni ya Bunge sehemu ya 11, Ibara ya 121, 122, 123, 124, 125 na 126 na pia kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 146 A.
Sehemu ya 11 ya Kanuni ya Bunge, Ibara ya 121 inaeleza kuwa mbunge yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya hoja ya kumshtaki Rais kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kupitia azimio la Bunge kwa mujibu wa Ibara  ya 46 A ya Katiba ikiwa inadaiwa kwamba Rais; ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja katiba au sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Lissu alisema atakusanya saini za wabunge kuunga mkono hoja yake ambayo ni asilimia 20 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Wabunge wote kikatiba ni 357.
Julai 13, mwaka huu wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani katika Wizara ya Katiba na Sheria bungeni, Lissu alisema uteuzi wa majaji umegubikwa na ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema baadhi ya majaji walioteuliwa hawana sifa, uwezo na kwamba hawakufaa kufanya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha Bunge kuiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan Ngwilizi kumhoji ili athibitishe kauli yake.
Alisema wakati akihojiwa na kamati hiyo, pamoja na nyaraka nyingine, aliwasilisha nakala ya ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuchunguza uteuzi wa majaji nchini.
Alisema ripoti ya kikosi kazi hicho kilibaini kuwapo majaji ambao hawana sifa ya kufanya kazi hiyo, lakini Rais Kikwete ameshindwa kuwaondoa kazini.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, alisema hali ya Mahakama ni mbaya, kwani kuna majaji wawili ambao waliwahi kukamatwa kwa rushwa wakiwa mawakili, lakini wakateuliwa kufanya kazi hiyo.
Alisema baadhi ya majaji hawana uwezo hata wa kuandika hukumu kutokana na kutojua vyema lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo inayotumika katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Alisema ili mtu aweze kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu lazima awe na elimu ya shahada ya kwanza ya sheria, awe ametumikia miaka 10 mahakamani na anayechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani lazima awe ametumikia miaka 15 mahakamani.
Mbali ya kueleza hayo, Lissu alisema kwamba alitoa pia katika kamati hiyo, ushahidi unaoonyesha kuwa kuna jaji mmoja wa Mahakama Kuu ambaye hawezi hata kuandika sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka... “Kama jaji hawezi kuandika hata sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka, tunaweza vipi kuwa na Mahakama  inayotenda haki?”
Alisema kuna jaji mwingine ambaye ameongezewa mkataba wa kufanya kazi mara ya tatu kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Alisema kwa mujibu wa Tume ya Mahakama, hakuna jaji ambaye anaweza kufanya kazi kwa mkataba kwa vipindi vitatu.
Kama Lissu atachukua hatua hiyo, itakuwa ni mara ya pili kwa mbunge kuwasilisha bungeni hoja ya kutaka kumwajibisha kiongozi wa juu serikalini.
Mara ya kwanza alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe katika Bunge lililopita alipokusanya saini za wabunge kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitaka awawajibishe baadhi ya mawaziri waliokuwa wametajwa kuhusika katika matumizi mabaya ya madaraka katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Rais Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza lake la Mawaziri hivyo kuzima hoja hiyo ya Zitto.

No comments:

Post a Comment