Friday, February 1, 2013

MAGAZETI YA LEO:Mbowe ambana Pinda bungeni

SAKATA la gesi limetua rasmi bungeni baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kuitaka Serikali iweke hadharani mikataba ya utengenezaji wa bomba la kusafirishia gesi hiyo kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ili kuondoa usiri uliogubika mradi huo.
Mbowe alitoa wito huo jana alipokuwa akimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda maswali bungeni katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu.
“Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kuwa vurugu za Lindi na Mtwara zimesababishwa na mawasiliano hafifu kati ya Serikali na wananchi, ikiwamo kauli za viongozi wa Serikali na CCM je, ni kwa nini Serikali isiwachukulie hatua za uwajibikaji watumishi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanaonekana dhahiri kuhusika,” alihoji Mbowe.

Kiongozi huyo wa upinzani alimtaka Waziri Mkuu kueleza ni kwa nini Serikali isiweke wazi mikataba yote ya gesi ili kuondoa hofu iliyojengeka kwa wananchi kwamba kumekuwa na hali ya ufisadi.

Akijibu swali hilo, Pinda aliwataka wabunge kutumia utaratibu mzuri wa kupata mikataba hiyo akisema haiwezekani ikawekwa hadharani.

Mbali na jibu hilo, Pinda alivitupia lawama vyama vya siasa akisema vimechangia kwa kiasi kikubwa mgogoro wa gesi mkoani Mtwara.
Licha ya juzi kueleza kuwa kulikuwa na mgogoro wa viongozi ndani ya mkoa huo pamoja na CCM, jana alikwepa swali la kutaka wahusika wawajibike na badala yake akasema suala hilo liko juu yake.

Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali lingine la Mbowe ambaye alimtaka Pinda kutoa kauli juu ya nani aliyesababisha mgogoro wa Mtwara uliosababisha maafa.

Hata hivyo, alitangaza neema kwa waathirika kwamba Serikali inaangalia namna ya kuwapunguzia gharama wale wote waliopatwa na matatizo hayo ikiwamo kuwalipa fidia.
“Vyama vya siasa vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kupotosha jambo hilo, ushindani wa chaguzi zinazokuja umejitokeza pia,” alijibu Pinda.

Kiongozi huyo alisema wanaofanya uchochezi huo wanafanya bila ya kujua kwamba unaweza kuwakumba watu wote wakiwamo hao wanaofanya hivyo.
“Tutalaumiana wengi lakini ni vyema kuweka mambo hadharani na kwamba ni hatari kufanya mambo kama hayo kwani amani ya nchi ni lulu ambayo ikipotea inaweza kuwa tabu kuipata.”

Alipinga hoja ya Mbowe kuwa Serikali inatekeleza majukumu yake baada ya shinikizo na maandamano ya wanasiasa.
Alilieleza Bunge kuwa wananchi wa Mtwara wanaweza kupoteza fursa nyingi kutokana na wawekezaji kuanza kuondoka wakikwepa vurugu na kukimbilia Msumbiji ambako kuna dalili za gesi pia.

Kamati ya Makinda yayeyuka
Jana, Spika wa Bunge Anne Makinda aliliambia Bunge kuwa Kamati aliyotarajia kuiunda haitakuwapo kutokana na ukweli waliokuwa wakiutaka kutoka Mtwara kuelezwa na Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment