Friday, February 1, 2013

Mzee Laiboni; Miaka 103, wake 40, watoto 113, wajukuu lukuki!

ASILIMIA 60 ya watu duniani huamini kuwa hadhi ya mtu kwenye jamii ni kuwa na fedha, magari au nyumba.
Hata hivyo , kwa Mzee Meshiko Mapi, Mmasai mwenye umri wa miaka 103, kwake maisha mazuri na yenye hadhi ni wake zake wengi, watoto, wajukuu na ng’ombe wengi wa kutosha.
Unapoingia katika eneo lake unamkuta mzee huyu akiwa  katika himaya yake ya kifahari, katika Kijiji cha Esilalee, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha. Himaya hiyo ipo katikati ya eneo la Miji midogo ya Makuyuni na Mto wa Mbu.                  
Magari yote ya abiria yanayopita  kijijini Esilalee kwenda maeneo mengine, yanakifahamu kituo  maarufu  cha kwa ‘Laiboni.’
Laiboni, ni jina  maarufu la Mzee Mapi na  yeye ndiye mmiliki wa kijiji hicho kwani wakazi wote wa kijiji hicho  ama ni watoto au wajuku zake.
Si hivyo tu, bali Shule ya Msingi Laiboni iliyopo katika kijiji hicho nayo ni ya kwake na  baadhi ya wanafunzi  wa shule hiyo ni watoto na hata wajukuu zake.  Kijiji hiki kimepambwa kwa mandhari yenye nyumba ndogondogo za msonge. Ni nyumba tatu tu kati ya hizo, ndizo zilizojengwa kwa matofali na kuezekwa kwa bati.
Nyumba ya  Laiboni, ambayo ni ya kisasa, ipo katikati ya kijiji, zizi la mifugo limejengwa mbali kidogo, kiasi cha hatua 100 kutoka zilipo nyumba nyingine.
Ingawa ni siku ya Jumapili, lakini kijiji hicho kimetawaliwa na ukimya mwingi. Shinini Mapiko Mapi, mtoto wa 82 wa Laiboni, ambaye ndiye mkalimani wangu anasema wanafamilia wengi wamekwenda katika shughuli zao, zikiwamo za kuchunga mifugo na nyinginezo. Karibu wakazi wote katika kijiji hiki hawafahamu Kiswahili, baadhi  wanayafahamu maneno machache na kuelewa lugha hiyo kwa kiasi kidogo.
Hata hivyo, Shinini peke yake ndiye anayeielewa  lugha ya Kiswahili ukilinganisha na wengine na yeye anakuwa msaada mkubwa kwangu, kama mfasiri.
Nzi, wadudu ambao hupenda mazingira yenye majimaji, maziwa au wanyama ndiyo wanaokukaribisha mahali pale, bila shaka wanasababishwa na wingi wa ng’ombe zaidi ya 2500  mali ya  Laiboni, ni kero kwa wageni na pengine hata kwa wakazi hao.
Unakutana na Laiboni, ameketi na watoto wake wa kiume 11, ambao ni sawa na timu ya mpira wa miguu.
Wengine wanacheza bao, baadhi wamejilaza huku wakiendelea kuwafukuza nzi waliokithiri.
Laiboni, mwenyewe ameketi kwenye kiti cha ngozi naye akifukuzana na nzi kwa kutumia usinga wa mkia wa ng’ombe.

No comments:

Post a Comment