Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alitoa kauli hiyo jana, baada ya RAI Jumatano kutaka kujua msimamo wake kutokana na kuhusishwa kuwa nyuma ya usaliti anaodaiwa kuufanya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Katika majibu yake hayo aliyoyatoa kwa njia ya mtandao, Zitto alisema wanaojaribu kumhusisha na suala la Mwigamba ni kawaida yao kupenda kumhusisha na mambo yasiyomhusu.
“Mwigamba ni Mwenyekiti wa chama wa Mkoa mwenye utashi wake wa kisiasa. Ana uwezo wa kusimama mwenyewe. Siyo kila mtu mwenye mawazo yake anatumika. Sasa hao wanaomtuhumu Mwigamba wao wanatumiwa na nani?” alihoji Zitto.
Kuhusu hoja kwamba sakata hilo la Mwigamba chanzo chake ni msuguano wa kuwania nafasi ya uenyekiti kati yake na Mbowe, Zitto alisema uchaguzi ndani ya chama haujatangazwa, kwa hiyo yeyote anayezungumzia kugombea au la anavunja kanuni za uchaguzi.
Katika hilo, Zitto alisema hahitaji mtu wa kumsemea, kwamba akihitaji uenyekiti wa chama atasema yeye mwenyewe.
“Nina sifa zote, siyo tu za kuongoza chama, bali kuongoza nchi. Nina elimu ya kutosha, nina rekodi ya kazi za kibunge kubwa kuliko wabunge takribani wote wa sasa, kwa miswada binafsi, hoja binafsi na hata kuibua masuala nyeti ya nchi.
“Uadilifu wangu hauna shaka, uzalendo wangu kwa nchi yangu ni wa kupigiwa mfano. Zaidi ya yote, najua kero za wananchi na changamoto zao. Sihitaji kusemewa na mtu. Nikitaka uenyekiti nitasimama mwenyewe,” alisema Zitto.
Zitto alisema kitendo cha kutaka kumhusisha na masuala yanayoendelea ndani ya Chadema na kuhusu sakata zima la Mwigamba, ni kutaka kuhamisha mjadala na kumtoa kwenye ajenda ya kuwafuatilia watu wanaodaiwa kuficha mamilioni ya fedha nje ya nchi.
“Kwa sasa nina kazi ya kuhakikisha mafisadi na wahuni ‘criminals’ walioficha fedha na mali nje ya nchi wanaibuliwa na kurejesha fedha hizo,” alisisitiza Zitto.
Kuhusu madai ya kuchunguzwa na chama chake kama na yeye ni mmoja wa wasaliti, Zitto alisema kuwa hizo ni mbinu za kumuondoa kwenye kazi anayofanya ya kupambana na ufisadi.
“Wanajua nikishika jambo siachi mpaka mwisho, hivyo wanajaribu kutengeneza uongo wanaouita uchunguzi. Watanzania wasipumbazwe na vituko vya siasa vinavyoendelea. Tuendelee kudai Katiba Mpya na kupambana na ufisadi. Kwa Wanachadema tuendelee kujenga chama kwenye kanda zetu. Chama kitakachochukua dola ni kile chenye mtandao mpana kwenda vijijini,” alisema.
Zitto aliwataka viongozi wenzake na wanachama wa Chadema kupunguza vikao vya majungu vinavyoishia kupigana na badala yake waende kwa wananchi wakafanye kazi, kwamba malumbano hayajengi chama.
Kwa upande mwingine, chama hicho kimeendelea kusisitiza kuwa madai yote yaliyotolewa na Mwigamba dhidi ya chama chao ni ya upotoshaji, uongo na ya kichonganishi.
Kwa mujibu wa tarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari Mwandamizi wa chama hicho, Tumaini Makene, wameshangazwa na hatua ya Mwigamba kuendelea kuvunja katiba ya chama kwa kutunga mambo yasiyokuwepo, badala ya kuwasilisha hoja zake kupitia vikao halali vya chama.
Alisema kwa kuwa Mwigamba amekiri mbele ya waandishi wa habari kuwa amevunja katiba ya chama na kukubali kuwa aliandika kwa kutumia jina bandia waraka na kuuweka kwenye mitandao ya kijamii, ni wazi hana lengo zuri na chama chao, hivyo apuuzwe.
No comments:
Post a Comment