Tuesday, December 3, 2013

Mwanamuziki Tabuley Hatunaye tena DunianiTabu Ley Rochereau, mwanamuziki maarufu na mwanzilishi wa mtindo wa rumba wa soukous akijulikana kama"Mfalme wa Rumba la Congo" ambaye alikuwa mmoja wa wanamuziki waliopendwa barani Afrika, amefariki Jumamosi katika hospitali moja mjini Brussels, Ubelgiji.
Mwanamuziki huyo akiitwa Pascal-Emmanuel Sinamoyi Tabu alizaliwa wakati wa utawala wa Wabelgiji nchini Congo mwaka 1937 au 1940, kutegemea na vyanzo vya habari, alikuwa akiumwa tangu mwaka 2008 akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi. Kiongozi wa bendi ya Orchestre Afrisa International alikuwa ni kiongozi mbunifu ambaye uimbaji wake uliunganisha sauti za muziki wa Kiafrika, Cuba,na mirindimo ya Caribbean, na aliimba bila kuchoka na kubandikwa jina la "Sauti ya Mwangaza."

Mwanamuziki Tabu Ley ambaye alikuja kushirikiana kimuziki na hata kimapenzi na mwanamuziki wa kike kutoka huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Mbilia Bel, alitikisa anga ya muziki wa rumba duniani, na hususan eneo la Afrika Mashariki na Kati.Muziki wa Tabu Ley unapatikana katika mamia ya santuri za LP. Miongoni mwa santuri hizo ni ile ya Ley, Ley, Seigneur Ley Rochereau. Pia kwa weledi mkubwa kazi zake zimekusanywa katika CD.
Kwa mfano mwaka 1987 alifanya ziara nchini Tanzania, wakiwa na Mbilia Bel na kutembelea mikoa kadha, ikiwa ni kusherehekea miaka kumi ya kuzaliwa kwa chama tawala cha CCM, nchini Tanzania.
Miongoni mwa vibao vilivyompa umaarufu mkubwa Tabu Ley ni Muzina, Maze, C'est comme ca la vie, selikutu, Ibeba, Nadina na nyingine nyingi.
Wapenzi wa muziki wa rumba, watamkosa Tabu Ley, lakini wataendelea kuburudika na nyimbo zake ambazo alizitunga katika uhai wake, akiwa mwanamuziki.

No comments:

Post a Comment