Monday, November 3, 2014

SIASA: Warioba mwiba. Poul Makonda kukutana na waandishi wa habari Protea Hotel ili kuzungumzia sakata hilo

  • Hoja zawaumiza CCM, Makonda aongoza vijana kumshambulia
  • Mdahalo wavunjika, polisi waonyesha udhaifu
  • Meseji za kupanga vurugu zanaswa, wanavyuo wahusishwa

HOJA mbalimbali za aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, jana ziliwafanya baadhi ya makada wa CCM kupandwa na jazba na kuzua vurugu kubwa katika mdahalo ulioitishwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kujadili masuala yaliyomo katika Katiba iliyopendekezwa.
Mdahalo huo ambao ulipangwa kuhutubiwa na baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilibidi uvunjike kutokana na vurugu hizo kubwa.
Mbali na kuvunjika kwa mdahalo huo, pia Jaji Warioba ambaye pia ni Makamu wa Rais mstaafu katika serikali ya awamu ya Pili, alishambuliwa kwa kupigwa na Katibu wa Uhamasishaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, pamoja na wafuasi wengine wa chama hicho.
Kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, aliwaeleza wananchi waliohudhuria mdahalo huo dhamira yake ni kupata ufahamu wa masuala yaliyomo katika katiba na yale yaliyoondolewa, pia kufikia uamuzi sahihi siku ya kupiga kura ya kukataa au kukubali katiba hiyo.
Mara baada ya Butiku kumaliza kuongea, alimkaribisha mtoa mada Jaji Warioba, ambaye alizungumzia masuala mbalimbali yaliyoboreshwa na kuondolewa.
Muda wote Warioba alipokuwa akizungumza, wananchi walikuwa wakimshangilia kwa makofi huku baadhi ya vijana waliopangwa kufanya vurugu wakiwa wanahimizana kuonyesha mabango yao waliyoyaandaa juu.

Vurugu zilivyoanza
Vurugu mdahalo wavunjikaWakati Jaji Warioba akizungumzia masuala mbalimbali, alilalamikia kitendo cha watu kumtumia Mwalimu Nyerere kama kinga ya kufanikisha masuala yao, huku akieleza kuwa kiongozi huyo mpaka anafariki dunia alikuwa akiamini katika azimio la Arusha.
“Laiti kama Nyerere angekuwepo asingekubali viongozi kuweka fedha nje ya nchi, kama Nyerere angekuwepo asingekubali viongozi kupewa zawadi na kuzificha majumbani mwao na kama Mwalimu Nyerere angekuwepo katika zama hizi…asingeruhusu maadili ya viongozi kukataliwa kuingizwa katika katiba,” alisema Jaji Warioba.
Kauli hiyo, iliamsha hisia za vijana waliokuwa upande wa kulia kwa Jaji Warioba wakiongozwa na Paul Makonda, ambao waliinua mabango juu, baadhi yakisomeka; Katiba iliyopendekezwa tumeipokea, tumeielewa, tumeikubali na tutaipitisha.
Mengine yaliandikwa; Fedha za magharibi haziwezi kubomoa nchi yetu, Katiba iliyopendekezwa tumeielewa na tunaiunga mkono. Kisha kuanza kushangilia na kuimba CCM…CCM…CCM.
Baada ya hali hiyo, watu walianza kushikana mashati na viti kuanza kurushwa ukumbini na baadhi ya watu, huku Makonda akimkimbilia Amon Mpanju, ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la Walemavu, kumfanya kuwa kinga yake kwa kujificha mgongoni mwake.
Muda wote huo, wajumbe waliokuwa wamepangwa kutoa mada katika mdahalo huo walikuwa wamekaa meza kuu huku baadhi ya vijana wakiwa wamewawekea ulinzi.
Wakati viti vikiendelea kurushwa ukumbini humo na wengine kushambuliana kwa makonde, mlinzi wa Jaji Warioba alimuondoa kiongozi huyo aliyepewa ulinzi wa ziada na baadhi ya vijana.
Hata hivyo, Makonda alitumia nafasi hiyo kujipenyeza na kisha kumrushia kibao cha mgongoni Jaji Warioba na vijana wengine waliokuwa karibu yake wakaamua kumshambulia kiongozi huyo.
Katika hali hiyo, mlinzi wa Jaji Warioba alijitahidi kuzuia mikono ya washambulizi na kisha kumbeba juu kwa juu kiongozi huyo na kumpeleka katika chumba cha watu maalum kwa ajili ya usalama.
Kitendo hicho cha Makonda kumshambulia Jaji Warioba, kiliamsha hasira za wananchi na kuanza kumshambulia huku kiongozi huyo wa uhamasishaji wa UVCCM akijitahidi kukimbilia katika moja ya vyumba vya wafanyabiashara hotelini humo kwa ajili ya kujiokoa.

Mpango wa kuvuruga mdahalo
Habari zilizopatikana kwa baadhi ya vijana ndani ya ukumbi wa mdahalo, zinaeleza kuwa waliofanya vurugu waliahidiwa kulipwa fedha baada ya kazi hiyo na kwamba, mkakati huo ulifanywa siku moja kabla ukiwahusisha baadhi ya wanavyuo.
Baadhi ya wanafunzi waliohusika wanatoka vyuo vya Mwalimu Nyerere Kigamboni na Chuo cha Usimamizi wa Maji na Maendeleo.
Baadhi ya wanafunzi hao walitumiwa ujumbe wa kwenda kufanya vurugu na mtu mwenye namba za simu 0656 501317 aliyejisajili kwa jina la Valence Kisima.
Katika ujumbe wake, Kisima aliwaandikia aliokusudia wakafanye vurugu kwamba; “Kesho Jumapili kuna kongamano Ubungo Plaza, mda (Muda) ni saa sita, nauli ipo kwa mshiriki mpe taarifa na mwenzio.
Ujumbe mwingine wa Kisima ulieleza; “But asivae rangi ya chama kijani wala njano coz 2kio ili ni maalum sana ntawapa maelekezo kesho saa tano nikija ukumbini.
Waliyosema awali
Awali kabla ya vurugu kuanza, Warioba alisema Watanzania hawapaswi kujivunia takwimu ya aslimia 81 ya masuala yaliyoingizwa katika katiba iliyopendekezwa, kwa kile alichoeleza masuala muhimu yaliyokuwa na nafasi ya kuleta mabadiliko yamewekwa pembeni.
Alisema mengi ya mambo yaliyoingizwa katika katiba hiyo ni yale mazuri yaliyochukuliwa katika katiba ya sasa huku masuala ya msingi yaliyopendekezwa na wananchi yakiwa yameachwa kando.
Aliongeza moja ya jukumu la tume aliyokuwa akiiongoza ni pamoja na kuchukua mazuri ya katiba inayotumika sasa na maoni mengine ya wananchi, huku akisema masuala ya tunu za taifa zilizoachwa na bunge maalum ni muhimu kwa ajili ya mabadiliko.
Butiku, alisema watazunguka katika mikoa ya Mwanza Mbeya na nchi ya Zanzibar, kwa ajili ya kufanya midahalo kama iliyofanyika katika maeneo mengine chini.
Alisema mdahalo wa jana, unapaswa kutafsiriwa kuwa ni wa watanzania na si wa makundi kama ilivyokuwa awali.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujua kilichomo ndani ya katiba hiyo, japo bado haijasambazwa kwa kiasi kikubwa na kwamba, kwa sasa inapaswa kujadiliwa na wananchi na siyo makundi.
“Tunataka mtaani katiba hii ijadiliwe pasipo kumuogopa mtu, hakuna kusimamiwa na yeyote wala chama chochote, katiba hii ni yenu ili kesho na kesho kutwa usije kumlaumu mtu au kulaumiwa na mjukuu wako kwa uamuzi mtakaofikia baada ya kura ya maoni,” alisema Butiku.
Humphrey Pole pole, aliwaeleza wahudhuriaji kuwa katiba iliyopendekezwa inapaswa kuangaliwa kwa umakini na kwamba, wananchi kuipigia kura ya hapana siyo dhambi.

kutokana na hali hiyo Kiongozi wa uhamasishaji wa wa UVCCM Poul Makonda amewaita waandishi wa habari asubuhi hii katika hotel ya porotea ili kuzungumzia sakata hilo lililolaaniwa na vijana wengi wa taifa kuwa kitendo hicho ni laana na waliofanya hayo hawatakaa salama.

No comments:

Post a Comment