Monday, March 11, 2013

Dawa za kutuliza maumivu na zinavyotumika kienyeji

Dawa maarufu za maumivu zilizozagaa katika maduka ya dawa nchini zinatajwa kuchangia ugonjwa wa kiharusi, moyo, vidonda vya tumbo na vifo vya ghafla, imebainika.
Imeelezwa kuwa watu wanaotumia dawa za kutuliza maumivu za Ibuprofen, Diclofenac na Diclopar mara kwa mara wapo katika hatari ya kupata maradhi ya moyo na kiharusi kwa asilimia 40 na hufa vifo vya ghafla.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Jiji la Dar es Salaam na viungo vyake umebaini kuwa madaktari wengi huwaandikia wagonjwa dawa hizo, zikiwa ndizo dawa maarufu za kutuliza maumivu.
Madaktari  na wafamasia hao waliulizwa kwa nyakati tofauti na Mwananchi, ni dawa zipi za maumivu wanazowaandikia mara kwa mara wagonjwa na wakazitaja kuwa ni Diclofenac, Ibuprofen, Diclopar, Paracetamol na  Tiroxam.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, kutoka Taasisi ya Moyo Tanzania, Ferdinand Masau anasema  kwa kawaida dawa zote zina madhara, ingawa hana uhakika iwapo dawa hizo zina athari kwenye moyo.
“Kwa ninavyojua dawa hizi zikitumiwa mara kwa mara zinasababisha michubuko tumboni na kusababisha vidonda vya tumbo,” anasema Dk Masau.
Mtaalamu wa Famasia ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema ana uhakika kuwa paracetamol (panadol) ikitumiwa kwa muda mrefu inaweza kusababisha matatizo katika ini na pia dawa hizo za maumivu huchochea vidonda vya tumbo.
“Paracetamol na Diclofenac zinaweza kusababisha ‘ulcers’ (vidonda vya tumbo) na baada ya muda mtu huweza kupata saratani ya ini, lakini kwa madhara mengine yaliyotajwa sina uhakika sana,” alisema famasia huyo.
Aidha, uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa wengi wanaotumia Diclofenac na Ibuprofen mioyo yao huwaenda mbio dakika chache baada ya kuzimeza.
Licha ya kuzungumza na madaktari, Mwananchi lilipita katika maduka kadhaa ya dawa na kugundua kuwa dawa hizo  huuzwa kwa wingi, tena bila ya cheti cha daktari.
Dawa  maarufu ya Ibuprofen inatajwa kuchangia kwa asilimia 18 shinikizo la damu na kiharusi.
Diclofenac inayopendelewa na watu wengi kwa kutuliza maumivu haraka  nayo imebainika kuchangia maradhi hayo kwa asilimia 51.
Kwingineko, utafiti uliofanywa katika nchi 51 duniani ikiwemo Tanzania umeonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 2.7 hufa kutokana na matumizi ya dawa hizi.
Dawa hizi aina ya NSAIDS kwa kawaida hutumika kutibu maumivu, uvimbe, maumivu ya mgongo, kichwa, homa, mafua na kushusha joto la mwili.
Takwimu zimeonyesha kuwa  matumizi ya dozi ndogo tu ya diclofenac hasa kwa  kutuliza maumivu kwa watu waliotoka kufanyiwa upasuaji  huchangia kwa asilimia 22  maradhi ya moyo.
Aidha, matumizi makubwa na ya mara kwa mara ya dawa hizo zinazoandikwa na madaktari zinachochea maradhi  ya moyo na kiharusi kwa asilimia 98.
Dawa ya Ibuprofen haina madhara kwa wale wanaotumia mara chache, lakini wale wanaotumia mara kwa mara wapo katika hatari kwa asilimia 78.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Patricia Mcgettigan anasema madaktari na wagonjwa wanahitaji uelewa zaidi kuhusu matumizi ya dawa hizi. Wapate uelewa juu ya hasara na faida za watumiaji wa dawa za maumivu.
Anasema watu wengi hasa katika nchi zinazoendelea hawana tabia ya kupima afya zao wakati mwingine hutumia dawa hizo wakiwa tayari na maradhi mengine na bila kuandikiwa na daktari hivyo kusababisha vifo.
Dk Mcgettigan anaongeza kuwa: “Watu wenye historia ya maradhi ya moyo, shinikizo la damu na kisukari wapo katika hatari ya vifo wanapotumia dawa hizi.”
Matumizi ya Diclofenac yametajwa kuwa ni mabaya zaidi ambapo zaidi ya asilimia 40 ya watu duniani huathirika kila mwaka.
Kwa maana hiyo katika kila watu 50 duniani, mtu mmoja huathiriwa na dawa hizo hasa kwa maradhi ya mshtuko wa moyo.
Imeelezwa kuwa mwanamke mdogo mwenye afya njema ana hatari ya kupata maradhi ya moyo kwa asilimia 0.1, lakini anaweza kupata maradhi ya moyo endapo atatumia moja ya dawa hizo mara kwa mara.
Matumizi ya dawa hizo
Mfamasia katika Kituo cha Kuzuia Magonjwa ya Kuambukiza (IDC), Aneth Wilbroad alisema tabia ya Watanzania kunywa dawa bila ushauri wa daktari lazima iachwe.
“Watu huua maini, figo, kwa sababu ya kunywa dawa bila mpangalio,” anasema Wilbroad.
 Anasema unywaji wa dawa za maumivu mara kwa mara bila vipimo unaweza kuzaa maradhi makubwa kama ini na figo ambavyo huchuja sumu mwilini.
“Si kila unapoumwa kichwa unywe dawa za maumivu, wakati mwingine maumivu husababishwa na msongo wa mawazo, njaa au kutokunywa maji,” alisema.
Anasema dawa si nzuri kwa asilimia 100 kwani zina madhara lakini zinatumika kwa sababu maradhi yapo. chanzo gazeti Mwananchi

No comments:

Post a Comment