Saturday, September 21, 2013

MASONGANGE NA MDOGO WAKE WAACHIWA HURU,

Mtanzania Agnes Gerald, maarufu Masogange, ameachiwa huru na Mahakama ya Kempton ya jijini Johannesburg, baada ya kulipa faini ya R30,000 (Sh4.8 milioni) kwa kosa la kubeba kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.
Wakati Masogange akitozwa faini hiyo mwenzake, Melissa Edward ameachiwa huru na mahakama hiyo, baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Msemaji wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai cha Afrika Kusini(Hawk), Kapteni Paul Ramaloko alisema Watanzania hao wameachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hawakubeba dawa za kulevya, bali kemikali aina ya ephedrine.
Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa, Melissa hana hatia kwa kuwa ilionekana kuwa amemsindikiza Masogange, ambaye alimwomba amsaidie kubeba mzigo huo.
“Mahakama iliona kuwa Melissa aliombwa tu kumsaidia kubeba baadhi ya mabegi, lakini hayakuwa yake. Mizigo yote iliandikwa jina la Agness Gerald na si Melissa,” alisema Kapteni Ramaloko.
Kapteni Ramaloko alisema, Melissa alijitetea kuwa hakuwa amesafiri pamoja na Masogange bali walikutana ndani ya ndege na Masogange alimwomba amsaidie kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa.
Kwa sheria za Afrika Kusini kubeba kemikali zozote ambazo zimepigwa marufuku ni kosa la jinai kisheria, hivyo mahakama iliamuru Masogange ahukumiwe kwenda jela kwa miezi 30 (miaka miwili na miezi mitano) au alipe faini ya R30, 000 (sawa na Sh4.8 milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye.
Alisema kutokana na kutomalizia kulipa fedha hizo ataendelea kubaki nchini humo hadi atakapomaliza kulipa nusu ya faini iliyobaki.
Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment